Hebrews 13

Huduma Inayompendeza Mungu

1 aEndeleeni kupendana kama ndugu. 2 bMsisahau kuwakaribisha wageni, kwa kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengine waliwakaribisha malaika pasipo kujua. 3 cWakumbukeni wale waliofungwa gerezani kana kwamba ninyi mmefungwa pamoja nao. Pia wakumbukeni wale wanaotendewa vibaya, kana kwamba ni ninyi wenyewe mnateswa.

4 dNdoa na iheshimiwe na watu wote, nayo malazi yawe safi, kwa kuwa Mungu atawahukumu wazinzi na waasherati wote. 5 eYalindeni maisha yenu msiwe na tabia ya kupenda fedha, bali mridhike na vile mlivyo navyo, kwa sababu Mungu amesema, “Kamwe sitakuacha,
wala sitakupungukia.”

6 fKwa hiyo tunaweza kusema kwa ujasiri, “Bwana ni msaada wangu; sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?”

7 gWakumbukeni viongozi wenu, wale waliowaambia neno la Mungu. Angalieni matokeo ya mwenendo wa maisha yao mkaiige imani yao. 8 hIsa Al-Masihi ni yeye yule jana, leo na hata milele.

9 iMsichukuliwe na kila aina ya mafundisho ya kigeni. Ni vyema mioyo yenu iimarishwe kwa neema, wala si kwa sheria kuhusu utaratibu wa vyakula, ambavyo havina faida kwa wale wanaozishika hizo sheria. 10 jSisi tunayo madhabahu ambayo wale wanaohudumu katika hema hawana haki ya kula vile vitu vilivyowekwa juu yake.

11 kKuhani mkuu huchukua damu ya wanyama na kuiingiza Patakatifu pa Patakatifu, kama sadaka ya dhambi, lakini miili ya hao wanyama huteketezwa nje ya kambi. 12 lVivyo hivyo, Isa naye aliteswa nje ya lango la mji ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe. 13 mKwa hiyo, basi na tumwendee nje ya kambi, tukiichukua aibu aliyobeba. 14 nKwa kuwa hapa hatuna mji udumuo, bali tunautafuta ule ujao.

15 oBasi kwa njia ya Isa, tuzidi kumtolea Mungu dhabihu ya sifa, yaani matunda ya midomo inayolikiri Jina lake. 16 pNa msiache kutenda mema na kushirikiana vile vitu mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu.

17 qWatiini viongozi wenu na kujinyenyekeza chini ya mamlaka yao. Kwa maana wao wanakesha kwa ajili yenu kama watu watakaopaswa kutoa hesabu. Watiini ili wafanye kazi yao kwa furaha, wala si kama mzigo, maana hiyo haitakuwa na faida kwenu.

18 rTuombeeni. Tuna hakika kuwa tunayo dhamiri safi na shauku ya kuishi kwa uadilifu kwa kila njia. 19Ninawasihi zaidi mniombee ili nipate kurudishwa kwenu upesi.

Maombi Ya Kuwatakia Baraka

20Basi Mungu wa amani, ambaye kwa damu ya Agano la milele alimleta tena kutoka kwa wafu Bwana wetu Isa, yule Mchungaji Mkuu wa kondoo, 21awafanye ninyi wakamilifu mkiwa mmekamilishwa katika kila jambo jema ili mpate kutenda mapenzi yake, naye atende ndani yetu kile kinachompendeza machoni Pake, kwa njia ya Isa Al-Masihi, ambaye utukufu una yeye milele na milele. Amen.

Maneno Ya Mwisho Na Salamu

22 sNdugu zangu, nawasihi mchukuliane na maneno yangu ya maonyo, kwa kuwa nimewaandikia waraka mfupi tu.

23 tNataka ninyi mjue kwamba ndugu yetu Timotheo amefunguliwa kutoka gerezani. Akifika mapema, nitakuja pamoja naye kuwaona.

24 uWasalimuni viongozi wenu wote na watakatifu wote. Wale wa kutoka Italia wanawasalimu.

25 vNeema iwe nanyi nyote. Amen.
Copyright information for SwhKC